Katibu Tawala Wilaya ya Mjini Juma Abdalla Hamad amewataka Masheha wa Wilaya hiyo kuhakikisha wanayatumia vyema mafunzo waliyopata kwa lengo la kuleta mabadiliko katika sekta ya Ardhi.
Akizungumza na masheha hao wakati alipokua akifunga mafunzo hayo ya marekebisho ya sheria za Ardhi huko katika ukumbi wa Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi Maisara ndg Juma amesema kuwa masheha wana mchango mkubwa katika jamii hivyo taaluma hiyo wanapaswa kuitumia ipasavyo kwani mchango wao utaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya sheria hizo.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeona wakati umefika sasa wa kuzifanyia marekebisho sheria za ardhi ili kwenda na wakati uliopo ndio maana ikaja na mpango huo kwa lengo la kumaliza migogoro ya ardhi nchini.
Akitoa mafunzo kwa Masheha hao Katibu wa bodi ya kudhibiti kodi za nyumba Ndg. Makame Sufiani kutoka kamisheni ya Ardhi alisema kua marekebisho ya sheria ni moja ya njia za uboreshaji wa kazi katika Taasisi tunazozitumikia kuendana na wakati uliopo hivyo mabadiliko hayo yamekuja mara baada ya kuona sheria nyingi za Ardhi zimepitwa na wakati na haziendani na huduma zinazotolewa.
Nao masheha hao wameupongeza uongozi wa Wizara hiyo kuweza kuutambua mchango wao na kuwapatia mafunzo kuhusiana na marekebisho ya sheria za ardhi kwa vile changamoto zinazohusiana na masuala ya Ardhi huanzia katika ngazi ya sheha hivyo wameahidi kuyafanyia kazi yale yote waliojifunza kwa mustakabli wa kuleta maendeleo ya Taifa.
Mafunzo hayo ya marekebisho ya sheria za Ardhi yameandaliwa na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makaazi na kuwashirikisha masheha wa Wilaya zote kwa awamu tofauti kwa lengo la kukusanya maoni na kufanyiwa kazi na kukamilika kwake kupitishwa katika Baraza la Wawakilishi.